Utangulizi Baada ya kufuatilia mjadala la Bunge Maalum la Katiba (BMK) ambapo kuliibuka hoja ya uingizwaji wa mfumo wa kimahakama, mahakama ya kadhi, katika mfumo rasmi wa kisheria wa Tanzania.
Mjadala huo ulichukua kasi miongoni mwa wajumbe na kuleta mgawanyo wa BMK katika makundi ya kupinga na kutetea hoja hiyo kwa misingi ya kidini. Kama raia niipendaye nchi yangu Tanzania nilivutiwa na mjadala na kutamani kujua kwa upana juu ya mambo yafuatayo:
1. Maana ya mahakama ya kadhi, shughuli zake na nguvu za kimamlaka za mahakama ya kadhi (Jurisdiction)
2. Historia ya uanzishwaji/urejeshwaji wa mahakama ya kadhi nchini Tanzania
3. Kujifunza kutoka kwenye uzoefu wa nchi zingine juu uwepo mahakama ya kadhi na nafasi ya Demokrasia na uhuru wa kuabudu
4. Je, kuna mantiki yoyote ya kimsingi ya uanzishwaji wa mahakam ya kadhi kikatiba (kidola)Kwa kutumia haki na uhuru wa kikatiba wa kutoa maono na kuelezea mawazo yangu, kutafuta na/au kusambaza taarifa pasipo kuzuiliwa na mipaka ya nchi n.k1.
Na kwa kutambua wazi na kwa bayana wajibu wangu wa kikatiba wa kuheshimu mawazo ya watu wengine, kuheshimu na kulinda haki zao na kutovunja sheria ya Tanzania.
Nimeona ni vyema nikajitafutia ukweli juu ya mambo haya kwa kurejea vyanzo mbalimbali vya taarifa ili niwe kwenye nafasi ya kisayansi ya ujenzi wa hoja pindi nijadilipo jambo hili. Ieleweke wazi ya kwamba nia yangu katika kujadili swala hili hadharani baada ya utafiti wa muda ni:
Mosi, kukuza ufahamu wa swala la kadhi miongoni kwa watanzania wenzangu – kwa njia ya kuwa na taarifa nyingi kadiri iwezekanavyo badala ya kuendesha mijadala kwa kukaririshwa. Pili, kutanua mjadala wa uanzishwaji wa mahakama ya kadhi kikatiba kwa kuuhusianisha na uhuru wa kuabudu na utangamano wa kitaifa.
Tatu, ni kujaribu kujenga misuli ya ustahimivu na uvumilivu wa kidini katika mijadala inayogusa maslahi mapana ya kitaifa badala ya kuwa na hisia na mihemko.
I. Maana ya mahakama ya kadhi, shughuli zake na nguvu za kimamlaka za mahakama ya kadhi (Jurisdiction) Ili kujenga uelewa mpana na wa kimantiki, ni vyema kuanza kwa kuyachambua kwa upekee maneno ya msingi ndani ya neno/dhana ya “Mahakama ya kadhi”. Mahakama ni mahala ambapo kesi na mashtaka mbalimbali husikilizwa na kuamuliwa; korti, Baraza.
2 Kwa kurejelea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mahakama ni “mamlaka yenye 1 Katiba ya Jamhuri ya Muungano (1977) ibara ya 18 (a), (b), (c) na (d) (Kwa Msisitizo wangu wangu) 2 TUKI. Kamusi ya Kiswahili Sanifu, 1981.
(Toleo la 2OO4)kauli ya mwisho ya utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano”3.
Pia wajibu wa mahakama ni “kutekeleza hukumu, amri na adhabu.”4 Ni katika msingi huo ndiyo unaweza kubaini ya kwamba msingi wa mahakama ni katika kutoa haki kwa binadamu, si tu kama chombo kingine, bali ndiyo chombo cha pekee na cha mwisho (final and conclusive).
Haki za binadamu zinazotolewa katika mikataba ya kimataifa kisha kuridhiwa na nchi husika hukosa nguvu za kiutendaji na kiutekelezaji iwapo hazitatungiwa sheria na kusimamiwa na chombo kiitwacho mahakama.
Iwapo mtu, (taasisi au jumuiya ya watu) akatokea kutoridhishwa na usimamamizi na utekelezaji wa sheria, atapaswa kukata rufani kwenye ngazi ya juu ya mahakama.
Hii ni sawa sawa na kusema “hakuna aliye juu ya mahakama”. Kwa hivyo basi, mahakama ni chombo adhimu kiasi hicho. Ni katika msingi huo wa uelewa wa mahakama ikanilazimu kujihoji maswali kadhaa katika kutaka kujua kuhusu mahakama ya kadhi:
Je, kuna chombo cha juu ambacho hupelekewa rufani zitokanazo na kutokuridhishwa na maamuzi ya mahakama ya kadhi? (Msingi wa pili wa swali hili nitaujadili hapo baadaye katika kipengele cha dhana ya kadhi) Ni nini hasa (haki zipi) kinachotekelezwa na kusimamiwa na mahakama ya kadhi? (Nia ya swali hili kutaka kuona “ombwe” lililopo baina ya mfumo wa sasa wa kimahakama na mfumo tarajali wa kikadhi).
Kimantiki, kama hakuna mapungufu yoyote kwenye mfumo wa sasa wa kimahakama hakuna haja ya kuanzisha mfumo 3 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (Toleo la 2OO5) Ibara ya 1O7 A.- (1), uk. 92 4 Rud. Ibara ya 15.- (2) (b)mbadala kikatiba (kidola).
Na kama kuna Ombwe, je, lapaswa kuzibika kwa njia ya mahakama ya kadhi pekee?
Ni nani hasa huguswa na maamuzi ya mahakama ya kadhi? Mambo ya msingi kuyatambua na kuyawekea Msisitizo katika uelewa wa dhana ya mahakama ni ile “mahakama ndiyo muhimili wenye wajibu wakusimamia na kutekeleza sheria.”
Kwa kurejelea Kamusi ya Lugha ya Kiswahili Sanifu, kadhi “ni hakimu wa Kiislamu mwenye madaraka ya kuamua daawa za kisheria” 5.
“Kutoka kwenye chanzo hicho hicho, daawa ni mashtaka yaliyofikishwa mahakamani ili kutolewa hukumu; kesi au mambo yanayoleta ugomvi au kutokusikilizana; utesi” 6 Sheikh Abdubakar Jabir al-Jazair anatupa mwanga zaidi katika kuewa juu ya dhana ya ukadhi asemapo: Ukadhi ni 1.
Kufafanua hukumu za sheria na kuzitekeleza 2. Miongoni mwa fardhi kifaya, kwa hiyo inamlazimu kiongozi wa nchi amuweke kadhi katika kila miji iliyo katika utawala wake atakaekuwa badala yake katika kufafanua sheria na kuwalazimisha raia kuitekeleza kwa kauli ya Mtume (s.a.w)… 3.
… ni kuttekeleza sheria ya Allah kwa niaba ya Allah na ukhalifa wa Mtume wake.7 Ni katika msingi huo basi ieleweke bayana ya kwamba, mahakama ya kadhi ni swala la kidini kwa kung’amua mantiki zifuatazo. Mosi, sheria inayosimamiwa na kutekelezwa kwenye aina hii ya mahakama huitwa “SHARIA” yaani sheria ya dini ya kiislamu. Pili, 5 TUKI, Kamusi la Kiswahili Sanifu, 1981 6 Rud 7 Sheikh Abdubakar Jabir al-Jazir. Minhajir Muslim:
Muongozo wa maisha ya Mwislamu, kitabu cha 3 Muamalat, 2OO3, uk. 3O8hakimu katika mahakama ya namna hii ni kiongozi wa kidini, yaani, uwepo wake kwenye nafasi ya u-kadhi ni misingi ya kidini (Kwenye mahakama za kawaida, hakimu anaweza kuwa na dini kama mtu binafsi lakini hiyo haitumiki kama msingi wa kupata nafasi husika).
Swala la ukadhi kubeba dhana ya udini ndani yake limejitokeza tangu serikali ya Tanganyika chini ya utawala wa Uingereza ilipofanyia marekebisho sheria ya
“The Native Courts Ordinance” ya mwaka 1929 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1936.
Ukisoma waraka wa serikali na 315/3 wa tarehe 1O/7/1936 kutolea maelezo juu ya sababu za kimsingi za kubadilisha jina la Mahakama ya Kadhi (Kadhi Courts) na kuwa mahakama ya Liwali (Liwali Courts) utakutana na maelezo haya “The post of kadhi implies more particulary the functions of a religious head of a Mohamedan community.
It would be better to use titles which as far as possible connote strictly secular duties, such as ‘Liwali and Akida” 8 Kwa tafsiri yangu,
“Nafasi u-kadhi huashiria moja kwa moja majukumu ya kiongozi wa jamii ya Muhamad (dini ya kiislamu). Ingekuwa ni bora kutumia vyeo ambavyo kwa kadiri iwezekanavyo vitaashiria majukumu ya kisekyula (yasiyo na muegamo kwenye dini/imani/itikadi yoyote ya kidini), kama vile Liwali na Akida” Katika uelewa huo mpana wa dhana ya mahakama na u-kadhi, ni muhimu kukumbuka yafuatayo: 8 Pius Msekwa, Historia ya Suala la Mhakama ya Kadhi Tanzania Bara, 2O11 (http://www.cms.ccmtz.org/index.php?newsid=125§ion=news&cmd=details)
Mahakama ndiyo chombo/muhimili pekee wenye mamlaka ya kusimamia na kutekeleza sheria (Kwa muktadha wa mahakama ya kadhi, sheria itakayosimamiwa ni sheria ya Kiislamu) Kadhi ni swala la kidini kwa uhalisia wake (nitadhihirisha hilo kwa kadiri ninavyoendelea kwenye makala haya) – kuanzia sheria inayotumika, mahakimu na utendaji wake Hivyo basi, haiyumkiniki kabisa ya kuwa wanaopigia chapuo (proponents) mahakama ya Kadhi wanapata nguvu na ujasiri wa kudai jambo la kidini
kikatiba/kiserikali/kidola? Ninatarajia kupokea ukinzani wa kihoja, kukosolewa na hata kurekebishwa… kwa misingi ya kihoja. Nakupenda sana Tanzania! Itaendelea….
Mwandishi wa Makala haya ni msomaji na mchambuzi wa mambo ya kiimani, kijamii na mwanafunzi wa kudumu.
255 754 917 764 kalekwajames@gmail.com