Baada ya Mchungaji Gwajima kukanusha ripoti zilizotolewa na Polisi kwamba Mtuhumiwa wa kumtesa Dr Ulimboka amekamatwa baada ya kutoa ushuhuda kanisani kwake, Kamanda wa polisi kanda maalum ya Dar es salaam Suleiman Kova amesema jeshi la polisi haliwezi kuingia kwenye malumbano na taasisi yoyote ya kidini kuhusiana na kukamatwa kwa mtuhumiwa wa kwanza kwenye kesi ya kutekwa na kuteswa kwa mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari Dr Ulimboka Steven kwa sababu ishu iko Mahakamani tayari.
Amesema taarifa zote zilizotolewa mwanzoni kuhusu Mtuhumiwa Getu Muhindi kwenda kwenye hilo Kanisa ni za kweli na uhakika.
Kova amesema daktari ndiye mwenye mamlaka ya kuthibitisha kama mtuhumiwa ana matatizo ya akili au ni mzima pamoja na kusisitiza kwamba ishu ya Dr Ulimboka isizungumziwe popote kwa sababu iko Mahakamani.
“sasa halizungumziki nje ya ulingo wa Mahakama, ukitaka kupata habari kuhusu shauri hili unakwenda Mahakamani siku ya kutajwa lakini nje ya hapa mtu yeyote akifanya hivyo anakiuka taratibu za katiba, mimi pia nafungwa mikono pamoja na kwamba nafahamu mambo mengi na ningeweza kutoa ufafanuzi mwingi sana lakini nimefungwa mikono yangu na utaratibu huo”