Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) ambaye pia ni ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Rulenge mkoani Kagera, Seveline Niwemugizi amesema, viongozi wa dini wana haki ya kuwaelimisha waumini wao waweze kujua kinachoendelea wanapoona kuna mambo hayaendi sawa katika jamii.
Askofu Niwemugizi ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro kuwataka maaskofu wasiwafundishe wananchi jinsi ya kupiga kura bali wawaache watumie haki yao ya katiba kupiga kura kulingana na utashi wao wenyewe.
“Nimeshangaa kusikia kuwa Waziri anasema viongozi wa dini hatuna haki ya kuwaambia waumini kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa, mbona Serikali imewaambia wananchi waipigie kura ya ndiyo, haki hiyo wameitoa wapi,” alihoji.
Namnukuu “Sisi ni viongozi wa dini hatuwezi kuwaona kondoo wa Bwana wanapotea halafu tukakaa kimya au kuwaacha, tutakuwa hatujatenda haki, lazima tuwaambie waweze kuondoka kwenye kundi hilo na waweze kujitambua,”
Niwemugizi alisema pia wanayo haki ya kuwaambia waumini wao kuipigia kura ya Hapana, Katiba Inayopendekezwa kwa sababu ni wajibu wao kufanya hivyo. Viongozi wa Dini ni viongozi wa jamii hawawezi kuona waumini wao wanapotea halafu wanakaa kimya maana kufanya hivyo kutasababisha waingie kwenye uovu.