Mwandishi James Kalekwa |
“Heri sifa njema, kuliko marhamu nzuri.” Mhubiri 7:1
Leo ninaomba kufanya mwendelezo wa hoja zangu juu ya Kwanini mimi humuita mzee Moses Kulola ni shujaa ukilinganisha na vijana wale maarufu wa zama zetu. Naomba kusisitiza kwamba nimejikita kwenye kanuni na wala si hisia za kidini na hivyo kila mwenye hekima anaweza kuuelewautendaji wa kanuni. Ndugu msomaji wa Uga wa Mkufunzi, unakumbuka harufu nzuri ya manukato ya watu watano uliokutana nao siku ya leo? Au jana?...Unaweza kutunza kumbukumbu ya harufu nzuri ya manukato hata baada ya miaka tisa?
HAPANA!!! Harufu nzuri ya malashi hujulikana pindi inapokuwepo tu, inapotoweka kujulikana kwake kunaisha. Ndiyo maana watu huenda kutafuta aina ya manukato ya kununua kwa kunusa kwasababu kumbukumbu ya manukato haipo tena!
Kwahiyo mtu mwenye manukato ya aina fulani ili tuendelee kumpa heshima ya manukato yake husika, anapaswa kuendelea kukaa nasi ili tusiisahau harufu nzuri ya manukato… Afadhali umenielewa!!!
Sifa njema hukaa… Kimsingi, sifa zote hukaa lakini sifa njema huendelea kuishi hata kama mwenye sifa amekwisha kulala mauti. Dunia nzima humkumbuka Nelson Mandela; nani asiyemjua Julius Nyerere?... Hao ni wanadamu wa kawaida kabisa na walitenda mazuri na walitenda makosa pia kwenye maisha yao, lakini kila majina yao yakitajwa mbele za watu ujue ni kwa sifa yao njema ndiyo wao hutajwa! Unamfahamu Idd Amin Dada mtawala wa kiimla wa Uganda?... Sifa yake ipo lakini imevunda!!! Kila akisemwa tu, ndani ya mioyo na mawazo ya wengi huibuka taswira mbaya juu yake.
Sifa ni wasifu wa muhusika na huo ndiyo msingi unipao Ujasiri kumwita mzee Kulola shujaa…
Kwa wasiomfahamu Dr. Moses Kulola ndiye mwanzilishi wa madhehebu ya Evangelical Assemblies of God Tanzania (EAGT) ambayo yamesambaa nchini Tanzania na nchi jirani.
Askofu mkuu Dr.Moses Kulola |
Kuna nyakati alikataa chakula ili autumie muda huo kuwaombea watu na kuombea nchi ya Tanzania…
Amehatarisha maisha yake: afya yake, uhai wake, mahusiano yake n.k ili kuona SHALOM ikitimilika kwenye maisha ya watanzania!
Maraisi wote wa nchi hii wanamtaja kuwa ni moja ya viongozi ambaye alikuwa ni mkweli SANA! Badala ya kuzungumza nyuma ya pazia alienda moja kwa moja kwa raisi husika na kuzungumza naye…
kama ni maonyo alitoa, kama ni kutia moyo alifanya hivyo na katika yote hayo aliwaombea na kuombea utawala husika! Ndiyo yake ilikuwa ni ndiyo na hapana yake ilikuwa hapana!
Viongozi wngi uwaonao sasa wa makanisa ya pentekoste na harakati ya Injili za uamsho hapa Tanzania wengi wamezaliwa, wamelelewa au wana uhusiano na kazi kubwa aliyoifanya mzee Kulola!
Kwakuwa hata sasa kila nikitembea ninaona mabango ya EAGT, ninasikia na kuwaona watu waliofanywa kuwa bora na kazi ya mzee huyu. Kwakuwa kila nikitazama huku na kule bado ninaona ni watu wachache sana hukubali kuyauza maisha yao kwaajili ya maisha ya watu wao… HII NI SIFA NJEMA!
Kwa misingi hiyo, marhamu nzuri ni nzuri lakini sifa njema ni HERI!
Tags:
James Kalekwa