Mwandishi James Kalekwa |
Majibu magumu kwenye maswali "mepesi": Kwanini humuita mzee Kulola Moses shujaa ukilinganisha na vijana wale?
Ulipotokea msiba wa askofu mkuu wa madhehebu ya EAGT Mzee Moses Kulola, kama ilivyo ada huwa kuna namna nyingi za kupokelewa kwa msiba, mathalani watu hutaka kumjua marehemu alikuwa ni nani kwenye nini? Alifanya nini wapi? Ameacha nini kwa nani? Lau kwa uchache na kwa msukumo tofauti, lakini hoja yangu ni kwamba wasifu wa marehemu hupanda chati siku mwili wake ukisubiri kurudi mavumbini...
Katika zama hizi za taarifa, kila mtu hujitafutia taarifa kutoka kule ajuako ili anapozileta kwenye kadamnasi ya mtandaoni naye afahamike "wamo" kwenye mambo ya kijamii... Wengine huvielekea vyanzo sahihi na wengine hujikuta kusini mwa taarifa na huambulia taarifa tepe tepe - zisizo na ukweli ndani yake! Almaarufu "Habari nyepesi nyepesi".
Yote tisa, kumi, huwa kuna makundi ya jamii ambayo hujipambanua kumfahamu marehemu na hivyo huomboleza kwa maandishi, huhudhuria msibani, na kwa zama hizi za taarifa, watu hawa hutafuta namna ya kuvuta usikivu wa watu juu ya marehemu... Hubadili picha za utambulisho kwenye mitandao ya kijamii na mambo kadha wa kadha!
Baada ya kifo cha mzee Kulola, rafiki yangu mmoja (rafiki kimtandao tu) ambaye huwa ni mchambuzi na mpembuzi yakinifu wa mambo mtambuka na yaibukayo katika jamii alinifuata pembeni, si mbele ya halaiki (inbox) akaniuliza "maswali ya kunifikirisha" ili tufanye mjadala au niache "ushabiki" wangu juu ya Moses Kulola... Maswali yalikuwa hivi:
1. WHO is this old folk, Sir. Dr. Moses Kulola that you celebrate his life?
2. J.K you are an open-minded friend, so be careful that you are not ensnared in the religious extremism. Hope this is not offensive, is it?
3. Does he amount to the fame of ***? (Hapo kuna majina ya vijana wawili maarufu waliokwisha kufariki dunia)
Hayo ni baadhi ya maswali ya ndugu yangu mpembuzi yakinifu... Kuna jambo alilisisitiza sana kwenye maswali yake. Alitaka sana kumlinganisha mzee Kulola na vijana wawili maarufu waliofariki kwa nyakati tofauti na vifo vyao kuchukua nafasi ya juu sana kwenye vichwa vya habari za Tanzania...
Ashukuriwe Mola lau kwa punje ya hekima alonijalia ya kujua "kutofanya maamuzi, kutotoa ahadi, au kutoa jibu ambalo ningependa nikumbukwe kwalo ilhali nikiwa kwenye hali ya hisia mchanganyiko."
kwahiyo niliishia kumshukuru rafiki yangu na kumuahidi kumpatia majibu ya kurudhisha kwa maswali yake mengi sana, ambayo aliendelea kuyaorodhesha hasa kipindi cha ukimya wangu...
Yapata maswali 50 hivi tena kwa kimombo!!! Wakati ninaendelea na uandaaji wa majibu yangu ya umakini ghafla ukatokea msiba wa Dr. Sengondo Mvungi, basi nikapata upenyo wa kumwelewesha jambo huyu ndugu yangu... Nikahariri maswali yake na kumrejeshea yakiuliza kuhusu Dr. Mvungi! Kisha msiba wa Dr. Mgimwa, nami nikafanya vivyo hivyo.
Naomba kupitia uga wa mkufunzi nitumie fursa hii adhama kuweka kumbukumbu sawa sawia kwa faida ya mpembuzi yakinifu na kila asomaye.
1. "Heri mwisho wa neno, kuliko mwanzo wake." Mhubiri 7:8
Katika kutafakari kwangu nikakumbuka sana moja ya hekima za mwenye hekima mkubwa kuwahi kuishi ulimwenguni Mfalme Sulemani. Kwa msingi wa hekima hiyo, jambo hupimwa kutokana na jinsi lilivyohitimishwa.
Neno laweza kuanza vyema, laweza kuanza kwa mafanikio lakini mwisho wake ukawa kinyume kabisa na kusudi la awali.
Naamini kwa akili na ufahamu wa kawaida kabisa tunaafikiana na ukweli kwamba kwenye mchezo wa riadha haijalishi umeanza kwa kasi kiasi gani, umewavuka watu wa ngapi njiani, umekuwa na mwanzo wenye kufurahisha kiasi gani lakini TUZO hutolewa MWISHO wa mashindano na ni kutokana na namna washindanao walivyomaliza riadha.
Vivyo hivyo kwenye mpira wa miguu na michezo mingine, mwisho huamua mshindi!
Sasa nirejee kwenye kujibu maswali na hoja. Vijana aliowataja ndugu mpembuzi yakinifu, kijana muigizaji maarufu wa filamu za Kiswahili aliyeleta "mapinduzi" kwenye tasnia hiyo na kijana mwingine mwanamuziki maarufu sana na bingwa wa "mitindo huru" kila mmoja aliyaishi maisha yake kisha akafariki kwa wakati wake.
Nianze na yule kijana wa filamu... Ukiunganisha nukta (connect dots) utagundua na kujifunza mambo kadhaa! Akiwa kwenye kipindi kimoja cha televisheni, kipindi maarufu sana, kijana huyo alikiri na kukanusha (kutangaza msimamo wake) juu ya mambo mawili yaliyoibuliwa na mtangazaji:
• Utumizi wa vileo
• Mahusiano ya kimapenzi
(Naomba niweke wazi mapema kabisa, sijaribu kumuhukumu mtu ila ninaunganisha nukta.)
Kijana huyu kwasababu anazozijua yeye aliamua kujipambanua kuwa ni kijana asiyetumia kileo na mcha Mungu.
Alikataa kata kata juu ya utumiaji wa kileo kwamba yeye si mtu wa namna hiyo. Lakini pia alitanabaisha kuwa yeye si mtu mwenye mahusiano ya kimapenzi na binti mwingine yeyote!
Hata hivyo, mazingira ya kifo chake yanakinzana KABISA na kijipambanua kwake.
Vipimo vya kitabibu na mazingira yalionyesha utumizi wa kileo na ushahidi wa ndugu wa karibu na wa kimazingira unaonyesha si tu mahusiano ya kimapenzi lakini pia chanzo cha kifo ni wivu wa kimapenzi!
Kijana alikufa katika mazingira hayo na juhudi za kufunika kombe zilifanyika sana lakini kama wasemavyo "la kuvunda halina ubani." mambo yalikuwa yamevunda tayari!
Kisha tuje kwa huyu kijana maarufu wa muziki... Mazingira ya kifo na maneno ya marafiki zake wa karibu yanadhihirisha kwamba naye alikufa kwenye mazingira ya ulevi achilia mbali ile kashfa ambayo ubani mwingi ulifukizwa kufunika harufu ya uvundo - madawa ya kulevya!
Sasa, kwa mazingira hayo ya mwisho wa hawa ndugu bado tuna ujasiri wa kuvika ushujaa eti tu kisa walipamba vichwa vya habari nchini? au kwa vile vyombo vya habari vilichagiza haya na yale juu ya maisha yao?
Je, bado tu wenye ujasiri kuupima ushujaa kwa "umaarufu"... Kwa kadiri nijuavyo mimi si kila shujaa huwa maarufu tena huu umaarufu wa kupika.
Kwahiyo, kama tunahitaji kufanya mjadala zaidi kuhusu ushujaa wa Mzee Kulola (hasa kwa kumlinganisha na vijana maarufu) basi kipimo cha kwanza kiwe ni ulinganifu wa mwisho wao.
"Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake."
2. Ndiyo utakumbukwa, lakini ni kwa lipi?. "Heri sifa njema, kuliko marhamu nzuri." Muhubiri 7:1
Juma lijalo nitatandaa ndani ya uga kuelezea hoja yangu nambari mbili.