"Ninapomkaribia nasikia sauti ya mtu huyo ikisema kwa taabu; naomba msaada jamani… naomba msaada jamani, hivi ndivyo anavyoanza kusimulia Juma Mgaza Abdallah, mtu wa kwanza kumwona Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka baada ya kutekwa, kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Abdallah, anasema mara baada kumwona daktari huyo akiwa katika hali hiyo, alijaribu kumkokota kumtoa eneo hilo, lakini alishindwa kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo.
Baada ya hapo, aliamua kusubiri mtu mwingine apite eneo hilo ili amwombe wasaidiane kumpeleka Kituo cha Polisi Bunju.
Anasema muda mfupi baadaye aliona gari likija mbele yao, akalinyooshea mkono kulisimamisha. Liliposimama, akamweleza dereva hali aliyokuwa nayo Dk Ulimboka na kwamba anahitaji msaada wa haraka.
Abdallah ambaye hadi wakati huo alikuwa hamfahamu mtu ambaye alikuwa akimsadia kuwa ni kiongozi wa madaktari kutokana na sura yake kuvimba, anasema walimwingiza katika gari hilo na kumpeleka Kituo Kidogo cha Polisi Bunju.
Anasema, Dk Ulimboka wakati huo alikuwa akiendelea kuvuja damu katika baadhi ya majeraha yake huku akiwa hana suruali na kubaki na bukta tu, huku akizungumza kwa taabu.
Kituo cha Polisi Bunju
Baada ya kumfikisha kituoni hapo, walitoa maelezo namna walivyomwokota na kumsaidia kumfikisha hapo.
Polisi baada kumhoji Dk Ulimboka, aliwatajia namba ya simu ya rafiki yake aitwaye Dk Deo. Walipompigia na kumweleza tatizo hilo, aliamua moja kwa moja kwenda Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kutoa taarifa hizo na hatimaye kuandamana na watu kadhaa kutoka hapo akiwamo Mkurugenzi wake, Hellen-Kijo Bisimba.
Wawasili kituoni
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania wa kituo hicho, Onesmo Olengurumwa, anasema waliwafika Polisi Bunju saa 3:36 asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka akiwa amekalishwa kwenye benchi huku damu ikiwa imeganda kwenye majeraha mwilini.
Olengurumwa anasema waliwahoji polisi waliokuwa kituoni hapo kwa nini wakae na mtu aliyeumia kiasi hicho muda mrefu bila ya kuita gari la wagonjwa kumchukua ili kuwahi kupatiwa matibabu.
Olengurumwa anasema polisi walisema kwamba, walikuwa wanawasubiri ndugu zake wafike.
Baada ya muda mfupi, akiwa ameingizwa kwenye gari kupelekwa hospitali, Dk Ulimboka aliomba maji ya kunywa akisema ana kiu sana, lakini alipopewa, alikunywa kidogo akashindwa.
Anasema wakiwa njiani, alikuwa akilalamika kuwa anasikika maumivu makali huku akisisitiza kuwa tukio la kutekwa na kupigwa lilikuwa la kumuua.
"Jamani hawa watu walitaka kuniua walikuwa wamepanga kuniua," alisikika mara kwa mara akisema Dk Ulimboka wakati anapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu.
Maelezo ya Dk Ulimboka
Baada ya Dk Ulimboka kuokotwa aliweza kuzungumza na kurekodiwa muda mfupi baada ya kutolewa msituni na mazungumzo yake yalikuwa hivi;
“Nilikamatwa na watu hao usiku wa Jumanne nikiwa maeneo ya Leaders Club, Kinondoni na daktari mwenzangu baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja ambaye alidai kuwa anafanya kazi Ikulu.
“Kuna jamaa mmoja anafanya kazi Ikulu, kama siku tatu mfululizo alikuwa akitaka kukutana na mimi ila nilishindwa kukutana naye kwa kuwa nilikuwa na kazi nyingi na wakati mwingine mpaka usiku,” alisema Dk Ulimboka.
Huku akizungumza kwa taabu kutokana na mdomo wake kuvimba, alisema siku hiyo mtu huyo alimpigia tena simu na kumtaka wakutane.
“ Jana (Jumanne) alinipigia simu na nikamwambia daktari mwenzangu twende tukaonane naye, wakati huo alitueleza kuwa alikuwa maeneo ya Kinondoni Stereo,” alisema Ulimboka na kuongeza:
“Tulipofika maeneo hayo tukampigia simu na akatueleza kuwa alikwisha ondoka, baadaye tukamweleza sehemu tulipo mimi pamoja na mwenzangu.”
Alisema kuwa, wakati anakutana na mtu yule maeneo ya Leaders Club, hakuwa na amani.
“Kwa kweli siku ile nilivyoonana na mtu yule sikuwa na amani kabisa ya kukaa eneo lile,” alisema Dk Ulimboka.
Alisema kuwa wakati wakiendelea na maongezi ya kawaida, bado aliendelea kuwa na mashaka na mtu yule.
“Katikati ya maongezi nikaona ameanza kuzungumza na simu, kila tukitaka kuagana alikuwa akizungumza na simu, sijui nini kilikuwa kinachelewesha sisi kuagana,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:
“ Ghafla walitokea watu kama watano na kusema kuwa hawana tatizo na mtu yeyote katika eneo hilo isipokuwa mimi.
Wakati sijakaa sawa, waliniburuza hadi barabara ya lami kwa kuwa eneo hilo lilikuwa karibu na barabara.”
Aliongeza, “Nilipowauliza wananipeleka wapi, wakaniambia kuwa mimi nasumbua sana na nitajua hukohuko, waliniingiza katika gari jeusi, lakini halikuwa na namba. Niliwauliza kosa gani nimefanya? Hawakunijibu kitu na kusema, we twende utajua hukohuko.’’
Alisema alipokuwa ndani ya gari hilo watu hao walimpiga na kwamba walipofika maeneo ya Victoria, walichukua sweta nyeusi na kumfunga usoni, jambo lililomfanya ashindwe kuona kinachoendelea ikiwa ni pamoja na alikokuwa akipelekwa.
“Walinipiga mateke ya mbavuni, wakati mwingine walitumia vitako vya bunduki, kila nilipokuwa najaribu kuangalia ninapokwenda nilishindwa,” alisimulia Dk Ulimboka.
Alisema kuwa watu hao walimpeleka katika nyumba moja ambayo hakujua iko sehemu gani ambapo walimshusha na kuanza kumshambulia kwa mateke mfululizo kila sehemu ya mwili. Wakati huo, wote walimshinikiza awaambie nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari.
“Tangu saa sita usiku mpaka saa 9:00 alfajiri walikuwa wananipiga tu, kuna wakati nilijaribu kukimbia wakapiga risasi juu nikasimama na sikuweza kukimbia tena,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:
“Nilisimama, wakaendelea kunipiga, niliwasikia wakisema ama wanichome sindano ya sumu nife au kunikanyaga na gari. Baadaye wakaanza kuning’oa meno na kucha kwa kolea huku wakinilazimisha kusema nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari."
Alisema kuwa, watu hao walikuwa na bunduki kubwa ambayo hakuweza kuitambua ni aina gani.
“Waliniambia kuwa ninajua ninachokifanya hivyo wanaweza kunichoma sindano ya sumu nife au wanikanyage na gari nife,” alisimulia.
Dk Ulimboka alisema kuwa awali hakuwa na shaka na watu hao kwa kuwa alidhani ni polisi, lakini baadaye alishindwa kuwaelewa kwani watu hao walimchanganya.
“Sikuweza kuwatambua ila naweza kusema ni askari, walipokuwa wananipeleka niliwauliza mnanipeleka wapi na wakati huo nilikuwa sioni mbele ila ilikuwa kama maeneo ya Mwenge hivi,” alisema Dk Ulimboka.
Alisema kuwa baadaye alipoteza fahamu na hakuweza kuona chochote zaidi ya kusikia sauti za watu hao kwa mbali.
“Nilikuwa sioni na nilipoteza fahamu nikawa nasikia tu wakinibeba, gari lilitembea muda mrefu, sikujua ni wapi tunakwenda, kumbe ndio huko Mabwepande,” alisema.
Alisema kuwa walifika maeneo ya barabara ya vumbi na baadaye wakamshusha na kumbeba hadi msituni.
“Waliniburuza na kuniacha huko na muda wa saa kumi alfajiri ndipo nikazinduka na kuanza kujiburuza kuelekea barabarani ambako nilisaidiwa na mtu mmoja ambaye simtambui,” alisema Dk Ulimboka.