Makamu Askofu Mkuu wa kanisa EAGT Mchungaji John Maene |
Moja ya vikao vya wachungaji ndani ya kanisa la EAGT Mlimwa West , picha ya Maktaba |
Tetesi za kufukuzwa kwa makamu askofu huyo zilianza kuvuma mwezi September ambapo gazeti la jibu la Maisha katika toleo lake namba 417 katika ukurasa wa mbele lilimhoji Askofu huyo ambaye alielezea kushtushwa tetesi hizo
Wiki moja baadae vyanzo vya habari vingine toka ndani ya kanisa hilo vilidai kuwa kuna kikao cha dharura kilichoitishwa Dodoma kwa ajili ya kushughulikia suala hilo ambapo vilidai kuwa sababu za kutenguliwa askofu huyo ni sababu za kimaadili bila kuainisha ni maadili gani huku wakisema mambo yote yatakua hadharani pindi uongozi wa juu utakapoamua kuachilia kwa vyombo vya habari
Vyanzo hivyo vilisema kikao hicho kilichofanyika Dodoma kilikua na ulinzi mkali wa askari polisi walioelekezwa kutambua waliohitajika kuingia kwenye kikao hicho.
Lango kuu la Kanisa la EAGT Mlimwa West |
Muonekano wa kanisa EAGT Mlimwa West ambapo vikao vya wachungaji hufanyika humo |
Askofu Mkuu wa EAGT Brown Mwakipesile |
Katika Mahojiano na gazeti la Jibu la Maisha kwa njia ya simu Askofu Mwakipesile aliwataka waumini wa kanisa hilo pamoja na wachungaji kuwa na subira mpaka hapo uongozi utakapotoa tamko kuhus jambo hilo.
Katibu Mkuu wa kanisa hilo Mchungaji Mwizarubi alipohojiwa kuhusu suala hilo hakutaka kuzungumzia suala hilo akidai kuwa yeye sio msemaji , mwenye kuzungumzia hilo ni askofu mkuu
Katibu Mkuu wa kanisa hilo Mchungaji Mwizarubi |
Akiongea na gazeti la Jibu la Maisha kwa njia ya simu kwa shida Makamu Askofu huyo Mchungaji John Maene alisema alipata Mshtuko tangu atoke katika kikao hicho cha Dodoma.
Mchungaji huyo mwenye umri wa miaka 70 alikiri kufukuzwa Uaskofu , Uchungaji na Uongozi wa kanisa hilo kwa kosa alililosema kuwa ni la mtu kutoa unabii na maono kumhusu.
Mchungaji Maene alidai kuwa kabla ya kikao hicho cha Dodoma aliwahi kuitwa katika kikao kilichohusisha Viongozi wa Kanda na Maaskofu wa Majimbo mwezi Septemba mwaka huu kujieleza.
“Ndugu mwandishi ,tuliitwa wote katika kikao hicho mimi na Yule Mchungaji aliyedai kuona maono kuhusu mimi kukiuka maadili ya kiroho, wakati nilipotakiwa kujieleza nilipata mshtuko wa moyo na kushindwa kuongea” alisema Mch Maene na kuongeza
“ Ndipo Viongozi hao walipotumia mwanya huo huo na kuendesha kikao hicho kwa upande mmoja na kutoa maamuzi ya kunifukuza kabisa ushirika wa kanisa hilo”
Akizungumzia kuhusu kikao cha Dodoma kilichofanyika wiki iliyopita alisema kuwa vilifanyika vikao mara mbili kilichowakutanisha viongozi wa wa kanda na cha pili cha viongozi wote wa majimbo na kanda
Alisema katika kikao cha viongozi wa kanda waliitwa wote kati yake na yule mchungaji aliyedai kuona maono na wote walitoa maelezo yao na kutoka nje, lakini kikao kilichohusisha viongozi wote wa majimbo na kanda hakuitwa
“Kikao hicho kilichohusisha vingozi hao wa kanda na majimbo kilisikiliza maelezo ya upande mmoja na kupiga kura ya kufukuzwa kwangu wakati huo mimi nilikua nje” alisema
Mimi niliilishia tu kupewa kupewa taarifa ya kufukuzwa Uchungaji na Uaskofu
Akizungumzia kuhusu tuhuma dhidi yake alisema kuwa ni mambo yaliyotokana na ndoto , maono na unabii kutoka kwa mchungaji mmoja wa kanisa huko Geita aliyedai kumuona akikiuka maadili ya kiroho.
Aidha alisema kuwa pamoja na kufukuzwa hajapewa barua yoyote mbali na kuelezwa tu na baadhi ya washirika wa kikao hicho kuwa amefukuzwa.
“Ndugu Mwandishi najua haya yanatokea sasa ni vita tu vya kiroho kwani nimekua mchungaji wa kanisa hili la EAGT Bugando tangu mwaka 1990 wakati Moses Kulola akiwa bado yuko hai na sikuwahi kupata tuhuma yoyote'' alisema maene akisikitika
“Naomba uniache nipumzike najisikia vibaya moyo unanienda mbio, mpaka sasa nimepigwa na butwaa sijajua nitafanya nini baada ya maamuzi haya nitawajuza” alisema mchungaji Maene na kukata simu