JUKWAA la Wakristo Tanzania (TCF), limeendelea kushikilia msimamo wake wa kuwashinikiza waumini kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa |
Askofu Dk. Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania |
Limesema Katiba Inayopendekezwa imefika hapo ilipo kwa njia ya ubabe na kukosa uadilifu.
Tamko la umoja huo lililotolewa jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet, limesema wao hawana hasira kama ambavyo watu wengine wamekuwa wakitafsiri.
Kauli hiyo inaonyesha kujibu kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Machi 28, mwaka huu alipokutana na viongozi dini wanaounda Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na viongozi hao, Rais Kikwete alisema msimamo wa TCF wa kuwataka waumini wao kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa ni wa hasira, pia usiokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.
Rais Kikwete alikuwa akizungumzia tamko la TCF la Machi 12, mwaka huu lililowataka waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kuipigia kura ya hapana Katiba hiyo.
Jukwaa hilo lilitaja sababu za uamuzi wake huo ni Muswada wa Mahakama ya Kadhi kukiuka misingi ya taifa kuwa na Serikali isiyo na dini, na kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa kuweza kusababisha mgawanyiko.
Katika tamko lake la jana, maaskofu hao wamesema kwa kuwa utafiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi ni vema Serikali ikaacha kujadili.
“Sisi maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tunatamka kwamba matamshi ya Rais Kikwete wakati akihutubia watu aliowaita viongozi wa dini Machi 28, kuwa Mahakama ya Kadhi ni ya Waislamu wenyewe na Serikali haitajihusisha wala kugharamia, yanakinzana na kile kinachoendelea bungeni na nje ya Bunge.
“Hapa tunajiuliza, endapo maneno ya rais ni ya kweli, mbona Bunge linaendelea kujadili kitu ambacho Serikali yake haitajihusisha wala kukigharimia?
“Kwa mantiki hiyo, tunamtaka rais aagize muswada huu uondolewe bungeni na usijadiliwe tena kwa kuwa utafiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, vinginevyo kuendelea kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba Serikali inajihusisha na itagharimia.
“Maaskofu tuliokutana hapa hatuna hasira na wala hatuongozwi na mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine wanavyotutafsiri.
“Tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi na sala, na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Maaskofu hao wamesema wako mjini Dodoma kufuatilia kwa kina muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ya mwaka 2014 unaopendekeza pamoja na mambo mengine, marekebisho ya sheria ya tamko la sheria za Kiislamu la mwaka 1964.
Wamesema muswada huo unaopendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi utawasilishwa bungeni leo kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo, wakati bado hoja zao za msingi walizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa Waziri Mkuu hazijajibiwa.
“Tangu tulipokutana Machi 10, mwaka huu tukatoa tamko letu kuhusiana na Mahakama ya Kadhi na Katiba Inayopendekezwa, tumekuwa tukiendelea kutafakari juu ya yale tuliyokuwa tumesema katika matamko yetu mbalimbali na jinsi amani na utulivu wa nchi yetu vinavyoendelea kumomonyoka siku zinavyokwenda.
“Kwanza tumeshangazwa na tabia ya viongozi wa Serikali ya kuitisha na kuendesha mikutano wanayodai ni ya viongozi wa dini, lakini isiyo rasmi.
“Machi 3, mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliitisha mkutano kupitia mchungaji mmoja ambapo hakuna hata kiongozi mmoja wa taasisi au kanisa aliyeshiriki.
“Jambo la kushangaza ni kile kilichotokea Machi 28, ambapo rais alishiriki kikao cha kikundi ambacho si rasmi, yaani Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam. “Tunasema kamati hiyo siyo rasmi kwa sababu haina baraka za viongozi wa ngazi za juu wa kidini wa mkoa huo na haina mwongozo wa kazi zake.
“Mikutano ya jinsi hii, kati ya Serikali na wale ambao imewaona kuwa ndio viongozi wa dini si sahihi kwani viongozi wa dini wana taratibu zao za kualikwa au kuwakilishwa katika mikutano na viongozi wa Serikali au wa dini au madhehebu mengine.
“Tunawashauri wanaohutubia na wanaoshiriki mikutano hii wajue washiriki hawana uwezo wa kuamua au kukubaliana na jambo lolote kwa niaba ya viongozi wao wa juu, na pia viongozi husika wa Serikali wasifurahi kwamba ujumbe wao umewafikia viongozi wa dini, kwani hao washiriki si wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa maamuzi au kukubaliana juu ya jambo fulani la kitaifa,” imesema sehemu ya tamko hilo.
Pamoja na mambo mengine, tamko hilo linasema kuhusu muswada wa Mahakama ya Kadhi imebainika walichokuwa wakikisema awali kitatokea kimeaanza kutokea bayana kutokana na yale yaliyotokea kwenye semina kuhusu mahakama hiyo ambapo baadhi ya wabunge walitofautiana na kutaka kupigana.
Hata hivyo, maaskofu hao wamesema endapo wabunge wa dini za Kikristo na Kiislamu watapigana na kisha baadaye wananchi nao wakafanya hivyo katika maeneo yao, Serikali itakuwa ndiyo chanzo cha mapigano hayo.
Maaskofu hao walioweka kambi mjini Dodoma, wamewataka viongozi wa Serikali kuacha kutumia vikundi visivyo rasmi kualika mikutano wanayodhani itakubalika na waumini wa dini hizo.
Wamesema mikutano yote ya jinsi hiyo itakayoitishwa ni batili na uamuzi wowote utakaofikiwa hautatambulika kwao.
Muswada Mahakama ya Kadhi waota ‘mbawa’ Wakati huohuo, Mwandishi Wetu Fredy Azzah anaripoti kutoka Dodoma kuwa muswada wa sheria ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi iliyotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, imeahirishwa. Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa uwasilishwaji wa sheria hiyo umesitishwa hadi itakapopangwa tena.
“Sheria hii haitawasilishwa tena, shughuli nyingine zitaendelea na kuna miswada mingi tu imeahirishwa ambayo kutokana na muda haitawasilishwa kwenye kikao hiki ikiwamo ya habari,” alisema Dk. Kashilila. Alisema mkutano wa 20 wa Bunge hilo unaotarajiwa kuanza Mei, ni mahususi kwa bajeti, lakini wabunge wakiona inafaa wanaweza kubadili kanuni wakajadili miswada watakayoona inafaa.
Chanzo:Mtanzania