Mbunge wa kuteuliwa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ameitaka Serikali kuchukua uamuzi mgumu wa kuzuia mihadhara ambayo inakashfu dini nyingine na kudai kuwa ndiyo inayopandikiza chuki miongoni mwa Watanzania.
Mbunge wa kuteuliwa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia |
“ Ni lazima tufike mahali tusema mihadhara ya kidini sasa basi, tuizuie kwa gharama yoyote kama tuna nia njema na nchi hii,” alisema Mbatia na kuongeza:
Mbatia alisema kuna viongozi ambao hawana nia ya dhati katika kukomesha tatizo hilo la udini kwani hata katika simu zao za mikononi zina miito yenye kuonyesha imani zao za dini.
“Kiongozi mzima simu yako ikiita inasikika miito ya pepo toka pepo toka, ama mingine inasikika miito ya kaswida, unawaonyesha mfano gani wananchi unaowaongoza,”alisema Mbatia.
Alisema hali hiyo ikiachwa iendelee katika siku zijazo baadhi ya viongozi watajikuta wakishtakiwa kwenye Mahakama ya The Hague, Uholanzi kwa kuchochea mauaji.
Alisema amani katika nchi hii ni lazima ilindwe kwa gharama yoyote ile bila kujali wanaofanya hivyo wana imani gani za kidini.
Naye Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alisema ni lazima Serikali ionyeshe kwamba ipo na inafanya kazi kwa sababu vitendo vya uhalifu vinazidi kuwatisha Watanzania.
“Hakuna askofu ambaye anaweza kuunda kikundi cha kihalifu cha kuwadhuru Waislamu, wala hakuna Sheikh ambaye atafanya hivyo kwa lengo la kuwadhuru Wakristo, wanaofanya uhalifu hawatakiwi kuvumiliwa,”alisema Selasini.
source: Mwananchi