Tamko la Jumuiya ya Madaktari Tanzania kuhusiana na tume iliyoundwa na jeshi la polisi kuchunguza tukio la Dr ulimboka.
KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI TANZANIA
YAH: TAMKO FUPI LA JUMUIYA YA MADAKTARI KWA WAANDISHI WA HABARI LEO TAREHE 28.06.2012
Madaktari
wote hatuna imani na tume iliyoundwa na Jeshi la polisi nchini yenye
lengo la kuendesha uchunguzi juu ya kutekwa, kunyanyaswa na kupigwa
vibaya kwa Dr. Ulimboka Stephen na tunataka chombo huru kiundwe ili
kupata ukweli wa tukio hilo.
Pia
tunakemea na kuonya juu ya vitisho vyote vinavyotolewa na baadhi ya
watawala katika taasisi mbalimbali dhidi ya madaktari mfano Hospitali ya
Rufaa ya Dodoma, Bugando, Mbeya na kwingineko ambapo wametishwa na
kufukuzwa kwa kutumia mabavu.
Madaktari
tunazidi kusisitiza kuwa hakuna njia nyingine yeyote ya kusuluhisha
mgogoro huu isipokuwa ni kwa kutekeleza madai na hoja za msingi za
madaktari kwa njia ya mazungumzo ya dhati.
Madaktari
tumechoka kuona huduma za afya nchini zikizidi kudorora mwaka hadi
mwaka, Tumechoka kuona wagonjwa wakilala chini na watoto wakilala wanne
katika kitanda kimoja Tumechoka kuona msongamano mkubwa kwa wagonjwa
katika hospitali zetu huku kukiwa hakuna mpango wowote wa uboreshaji.
Tumechoka
kuona wagonjwa wakikosa dawa, vipimo sahihi na watumishi wa afya
wakifanya kazi katika mazingira magumu yanayoviza ubora wa huduma na
misingi ya taaluma. Kwa hiyo, kwa moyo wetu leo tumejitolea kutetea
uboreshaji wa sekta ya afya licha ya vitisho tunavyoendelea kuvipata.
Rai
kwa Madaktari; Madaktari wote kuwa watulivu katika kipindi hiki
kigumu, tunashukuru madaktari wote kwa ushirikiano na kuendelea na
mshikamano.
Imetolewa na Kamati ya Jumuiya ya Madaktari.