Wakati mama mzazi wa msichana anayedaiwa kutaka kujiunga na Kundi la Al-Shabaab, Tahliya Sadir akisema kuwa anamwachia Mungu suala la binti yake, babu na bibi yake wameonekana kushtushwa na taarifa hizo na kusema hawakuwahi kufikiria kama mjukuu wao angethubutu kufanya uamuzi kama huo.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Tahliya alisema: “Namwachia Mungu suala hili, siwezi kuchukua hatua zaidi ya hapa.”Ummul Khayr Sadir Abdulla, alikamatwa Machi 30 katika mpaka wa Kenya na Somalia, El Wak, Jimbo la Mandera kwa kile kilichodaiwa kutaka kuingia nchini Somalia ili kujiunga na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.
Bibi na babu wa binti huyo, Masoud Salim na Asha Saleh ambao wote ni walimu walisema hawakufikiria kama jambo hilo lingetokea katika familia yao na kuongeza kuwa wanaamini ni suala la utoto tu.
“Sisi hii taarifa tumeipata kupitia vyombo vya habari” aliongea bibi huyo akitokwa machozi.
Bibi huyo alisema familia nzima ina wasiwasi mkubwa kutokana na ukubwa wa shutuma hiyo inayomkabili mjukuu wao na hawajui mwisho wake.
Naye, Masoud Salim alisema anaamini kuwa mjukuu wake anajua anachokifanya kwani mara ya mwisho, aliwaaga anakwenda masomoni Sudan ambako yeye na dada yake Sumaiya wanasomea fani ya udaktari.
Salim alisema baba na mama yake Ummul- Khayr wako nchini Kenya kufuatilia suala hilo.
Hata hivyo, Mwananchi lilipozungumza na mama yake Ummul Khayr, Tahliya alikataa kusema yupo wapi kwa wakati huo.
Ummul-Khayr ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, Sudan alikamatwa nchini Kenya akiwa na wenzake wawili raia wa Kenya, Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir.
Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athuman alisema bado wanasubiri majibu kutoka kwa polisi wa Kenya ili kuendelea na taratibu za kumrudisha msichana huyo nchini.
“Tumeshangaa hatujajibiwa lolote mpaka sasa, lakini wakitujibu taratibu zote zitafuatwa,” alisema DCI Diwani.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya alisema, ofisi yake imehakiki uraia wa msichana huyo na kujiridhisha kuwa ni Mtanzania.